Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania ‘BFT’ linahitaji zaidi ya Sh milioni 90 kwa ajili ya kambi na kuisafirisha timu ya taifa itakayoshiriki Mashindano ya Afrika Yaounde, Cameroon baadaye mwezi huu.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga, Sh milioni 17 ni kwa ajili ya kambi ya kudumu ya mazoezi ya timu hiyo iliyotarajia kuanza Julai Mosi hadi 25, ikihusisha chakula, vifaa vya mazoezi na vile vya mashindano pamoja na mahitaji mengine.

Mashaga amesema kuwa kiasi kingine cha Sh milioni 71 ni kwa ajili ya tiketi za ndege za kwenda na kurudi kwa mabondia nane, makocha wawili, viongozi wa BFT na mmoja wa serikali.

Mabondia wanaunda timu hiyo ya taifa ni pamoja na Yusufu Changarawe, Ilakunda Daniel, Davie Chanzi, Joseph Philipo, Sebastian John, Rajabu Chande, Mwalimi Saalum, Ramadhani Kitogo, Abadallah Mohamed, Hamadi Hashim wakati wanawake ni Grace Mwakamele na Zulfa Macho.

Mabonda hao walipatikana baada ya kufanyika mashindano ya majaribio kwa siku mbili kabla ya jopo la mabondia wa zamani na makocha kuwachagua mabondia hao kwa ajili ya mazoezi yanayoendelea kwenye ukumbi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mgulani.

Mashaga amesema kuwa kwa sasa shirikisho lake linatafuta fedha kuhakikisha timu hiyo inaingia katika kambi ya kudumu na kwenda katika mashindano hayo ya Afrika na kufanya vizuri.

Aidha, Mashaga amesema kuwa timu ya taifa ya ndondi mwezi Septemba itashiriki mashindano maalumu kwa ajili ya kusaka tiketi ya kushiriki Michezo ya Olimpiki itakayofanyika mwakani Paris, Ufaransa.

Haya hapa malengo ya Singida Fountain Gate
Ntibazonkiza: Nimerudi kufanya kazi