Uongozi wa Biashara United Mara umeonesha matumaini makubwa kwa kikosi cha klabu hiyo kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar utakaounguruma Juni 14.

Uongozi wa klabu hiyo umeonesha matumaini hayo, baada ya kuachana na Kocha kutoka nchini Burundi Vivier Bahati na kuwafukuza baadhi ya Maafisa wa Benchi la Ufundi mwanzoni mwa juma hili.

Kwa sasa kikosi cha Biashara United Mara kinafanya maandalizi ya kuelekea mchezo dhidi ya Kagera Sugar chini ya Mkurugenzi wa Ufundi Omar Madenge, huku Uongozi ukijipanga kumtangaza Kocha Mkuu mpya.

“Tayari tuna jina na Kocha Mkuu mpya ambaye ataungana nasi wakati wowote kuanzia sasa, tuna matarajio makubwa sana na Kocha huyo kwa sababu tunaamini atafanikiwa mpango wa kuibakisha timu yetu Ligi Kuu kupitia michezo iliyosalia kabla ya msimu huu haujamalizika.” Imeeleza taarifa ya Klabu hiyo.

Naye Mkurugenzi wa Ufundi Omar Madenge ambaye anakaimu nafasi ya Kocha Mkuu kwa sasa amesema: Tumebakisha michezo minne ambayo ni muhimu sana kwa sasa, tunaamini vijana watafanya vizuri ili tuweze kunusurika na hatari iliopo.”

“Ligi bado haijaisha, hakuna ambaye ameshashuka daraja hadi sasa, tunaamini michezo iliyobaki tutafanya vizuri kwa kupata alama zinazohitajika ili kujinusuru.”

Biashara United Mara hadi sasa ina michezo minne dhidi ya Kagera Sugar (Ugenini), Geita Gold (Ugenini), KMC FC (Nyumbani) na Azam FC (Ugenini).

Hadi sasa Biashara United Mara ipo nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa alama 24, baada ya michezo 26.

Dodoma Jiji FC yaihofia Geita Gold FC
Samatta awaita watanzania Kwa Mkapa