Uongozi wa Klabu ya Biashara United Mara umethibitisha kuwa timu yao itarejea katika Uwanja wa Karume mjini Musoma-Mara kwa ajili ya michezo yao mitatu ya nyumbani iliyosalia msimu huu.
Biashara United Mara ililazimika kuhamia jijini Mwanza na kutumia viwanja vya CCM Kirumba na Nyamagana, ili kupisha marekebisho katika Uwanja wa Karume ambao ulifungiwa na Bodi ya Ligi Tanzania Bara ‘TPLB’ kwa kukosa vigezo.
Mwenyekiti wa klabu hiyo Seleman Matasso amesema maboresho yaliyoagizwa kufanywa katika Uwanja wa Karume ili kukidhi vigezo yameshanywa, hivyo timu yao itarudi nyumbani.
Matasso amesema Uongozi wa klabu na baadhi ya wadau wa soka mjini Musoma-Mara umefanya jitihada kubwa kuhakikisha wanatimiza vigezo kwa kuuboresha Uwanja huo, ambao kwa misimu miwili iliyopita ulikua sehemu ya burudani.
“Tumeamua kurejea katika Uwanja wetu wa nyumbani, baada ya kufanywa kwa marekebisho na kuhakikisha michezo yote iliyosalia tunachezea hapa, niwaombe mashabiki wa soka mjini Musoma na maeneo mengine ya mkoa wa Mara kuungana na timu yao itakapokua nyumbani ili kuipa nguvu ya kubakisha alama tatu.”
“Kiukweli hatupo vizuri katika msimamo wa Ligi, na ushindani umekua mkubwa kutokanana kila timu kupambana ili kujihakikishia nafasi ya kubaki, nafasi tulionayo sio nzuri lakini tukishikamana kwa pamoja tutafanikiwa katika michezo yetu ya hapa nyumbani.”
“Tukishinda michezo mitatu ya hapo nyumbani kisha tukashinda michezo miwili mingine ugenini, kwa hakika timu yetu itakua salama na itabaki Ligi Kuu kwa msimu ujao, hivyo Mashabiki wanatakiwa kuwa kitu kimoja kwa ajili ya timu yao.” amesema kiongozi huyo
Biashara United Mara inayoshika nafasi ya 14 katika msimamo wa Ligi Kuu kwa kuwa na alama 23, itacheza nyumbani dhidi ya Young Africans, KMC FC na Dodoma Jiji FC.