Rais wa Marekani Joe Biden amezungumza kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed wakati na kuelezea wasi wasi wake kutokana na ghasia zinazoendelea nchini humo.
Aidha amelalamikia shambulizi la anga la hivi karibuni lililoua watu kadhaa kwenye kambi ya watu waliokoseshwa makazi jimboni Tigray.
Ikulu ya Marekani imesema kuwa viongozi hao wawili walizungumzia mikakati kuelekea kusitishwa kwa mapigano ambayo kwa kipindi cha takriban miezi 14 yameua maelfu ya watu huku mamilioni wakilazimika kutoroka makwao.
Sambamba na hayo yote Biden, amesisitiza upelekaji wa misaada nchini Ethiopia pamoja na haki za binadamu kwa wale walioathiriwa na mapigano, wakati kukiwa na wasiwasi kutokana na watu waliozuiliwa baada ya hali ya dharura kutangazwa nchini humo.