Urusi imempiga marufuku Rais wa Marekani Joe Biden kuingia nchini humo pamoja na maafisa wengine wakuu wa serikali yake.
Urusi iliweka vikwazo hivyo mnamo Jumanne, Machi 15, na kuwapiga marufuku vilevile Katibu wa Serikali ya Marakeni Antony Blinken, Katibu wa Ulinzi Lloyd Austin na Katibu wa Mawasiliano ya Ikulu ya White House Jen Psaki.
Utawala wa Urusi kupitia Moscow uliendelea na pia kuwapiga marufuku aliyekuwa Katibu wa Serikali ya Marakeni Hillary Clinton pamoja na mwanawe Biden, Hunter.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la CBS News, Urusi vilevile itafungia mali za wale wote waliotajwa katika orodha hiyo na wahusika wanadai hakuna kati yao aliyekuwa akipanga ziara ya kwenda nchini Urusi na waliongeza kuwa hawana akaunti za benki nchini humo na hivyo basi wataendelea na mipango yao bila kutatizika.
Marekani ilijiunga na jamii ya kimataifa kwa kutekeleza vikazo dhidi ya Urusi kufuatia hatua yake ya kuvamia taifa jirani la Ukraine.
Kando na vikwazo hivyo, kampuni nyingi za Kimerekani zimeacha kufanya biashara katika taifa la Urusi. Urusi nayo imeshikilia kuwa inapanga kuweka vikwazo zaidi katika siku za usoni kuwalenga wafanyabiashara na watu katika vyombo ya habari.