Mshambuliaji mpya wa Young Africans, Hafiz Konkoni amesababisha kushindwa kupewa nafasi kwa kiungo wa kimataifa wa Burundi, Gael Bigirimana, ambaye alirudi kikosini baada ya kuenguliwa msimu uliopita.
Konkoni, ambaye hana hata majuma mawili mazoezini, aliifungia Young Africans bao moja kwenye ushindi wa 6-1 dhidi ya Friends Rangers, Ijumaa (Agosti 04) iliyopita, akionyesha kuwa mtu sahihi kuziba nafasi ya Fiston Mayele.
Baada ya kuondoka kwa aliyekuwa nyota wa timu hiyo, Mayele, Young Africans iliingia sokoni kutafuta mrithi wake, lakini zoezi hilo likawa gumu kiasi cha mabosi kutaka kumwamini mshambuliaji kinda, Clement Mzize kucheza na Kennedy Musonda.
Lakini bado majadiliano yalikuwa makubwa na kuona kuna ulazima wa kuziba nafasi ya Mayele, wakati huo, Wananchi walikuwa tayari na nyota 12 wa kimataifa wanaotakiwa kikanuni, akiwamo na Bigirimana, ambaye alienguliwa kwa makubaliano katika dirisha dogo la Januari, akimpisha Mamadou Doumbia ambaye pia ameachwa.
Bigirimana alifika kambini Avic Town na kuanza mazoezi akiendelea kuutumikia mkataba wake wa miaka miwili, lakini ghafla alisimamishwa baada ya Young Africans kumpata Konkoni, kwani raia huyo wa Ghana litimiza idadi ya nyota 12 bila Bigi-rimana.
Watu wa karibu na Bigirimana, wameelza kuwa waliamua kukaa chini na Young Africans mwishoni mwa juma lililopita ili kuvunja mkataba jumla, baada ya awali kuambiwa wasubiri.
“Sasa tumechoka, alifanyiwa hivi msimu uliopita na sasa. Tumeamua kuvunja mkataba na tayari viongozi wa Young Africans wanalijua hilo na wanalifanyia kazi,” amesema mtu huyo wa karibu na nahodsha wa zamani wa Bigirimana.
Young Africans inaondoka Dar es Salaam leo Jumatatu (Agosti 07) kwenda jijini Tanga tayari kwa mechi za Ngao ya Jamii, ambapo mabingwa hao watetezi wataanza dhidi ya Azam FC keshokutwa Jumatano (Agosti 09).