Wajumbe wa Kikao cha ushauri cha Wilaya ya Biharamulo Mkoani Kagera DCC, kwa kauli Moja wamekubariana Wilaya hiyo kumegwa kwenda kuunda mkoa mpya wa Chato utakapotangazwa ili kuweza kusogeza huduma za kiutawala karibu na wananchi.
Maazimio hayo yamefikiwa na wajumbe hao ambao baadhi yao ni madiwani wa halmashauri hiyo chini ya mwenyekiti wa kikao hicho Kemirembe Lwota ambaye ni mkuu wa wilaya hiyo kilichofanyika kwenye ukumbi wa mkuu wa Wilaya, baada ya kuwahoji kama wanakubariana na kujiunga na mkoa mpya wa Chato.
Awali akisoma mapendekezo ya wataalamu kwenye kikao hicho Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Innocent Mkandala ameainisha faida za kujiunga kwenye mkoa mpya ni pamoja na kupunguza umbali kutoka Biharamulo kwenda Bukoba kilometa 178 na sasa Chato ni kilometa 73 tu.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Biharamulo magharibi Mhandisi Ezra chiwelesa amesema mkoa mpya utafungua fursa kwa Biharamulo kwani utaondoa mgongano wa maslahi wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato iliyokuwa ndani ya mikoa miwili, uwepo wa uwanja wa ndege ambao utafungua fursa za utalii na ujenzi wa barabara zinazounganisha Wilaya na Wilaya kwa kiwango cha lami hivyo wananchi kufanya biashara bila vikwazo vya miundombinu.
Ametaja manufaa mengine ya Mkoa mpya kuwa ni uwepo wa Hospitali ya Kanda, Bandari ya Nyamilembe ambapo magari makubwa yatakuwa yanapita Biharamulo kutoka nchi jirani na kufufua uchumi wa Wilaya na udugu wa Biharamulo na Chato kwani mpaka mwaka 2007 ilikuwa ni Wilaya Moja ya Biharamulo.