Serikali nchini, imesema imedhamiria kuwekeza kwenye Tiba Asili, baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kutoa kiasi cha Shilingi 2.7 Bilioni kwa ajili ya utafiti wa eneo hilo.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel wakati akizindua kituo cha Tiba Jumuishi cha Afrika Alama, kilichopo Kijiji cha Ngarenanyuki Wilayani Arumeru ambacho kinatumia mitishamba kutoa huduma za Tiba ya Afya.
Amesema, “Rais wetu Samia Suluhu Hassan ametoa Bilioni 2.7 kwa ajili ya utafiti kwenye eneo la Tiba Asili, Rais Samia ana nia ya dhati ya kuendeleza Tiba Asili, tuwatumie Tiba Jumuishi kuwajengea uwezo watu wetu ili nasi tuwe na Tiba Asili kama hii katika Hospitali zetu.”
Mapema mwezi Mei, 2022, Kaimu Mkuregenzi Msaidizi anayeshughulikia Tiba Asili na Tiba Mbadala Wizara ya Afya, Bi. Lucy Mziray aliwataka Waratibu wa Tiba asili kuwafundisha na kuwahamasisha waganga wa tiba asili na tiba mbadala juu ya ya sheria, miiko na maadili ya kazi wanazofanya katika jamii.