Serikali imetoa Sh. Bilioni 4.4 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za Radiolojia, jengo la kufua oksijeni pamoja na uboreshaji wa huduma za dharura na wagonjwa mahututi katika Hospitali Rufaa ya Jeshi Lugalo.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amesema hayo alipotembelea miradi hiyo ya ujenzi inayoendelea kutekelezwa ndani ya Hospitali hiyo Jijini Dar Es Salaam.
“Shilingi Bilioni 4.4 zimetolewa na Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya miradi ya ujenzi hapa Lugalo, lakini pia tumetoa zaidi ya Bilioni 4.8 kwa utekelezaji wa miradi ya afya kwenye Idara nyingine za Ulinzi na Usalama ikiwemo Jeshi la Polisi na Jeshi la Magereza,” amesema Prof. Makubi.
Ameongezea kuwa Wizara ya Afya itaendelea kushirikiana na Wizara na Taasisi nyinginezo kuboresha huduma za Afya.
Prof. Makubi ameipongeza Hospitali hiyo kwa usisamizi hodari wa miradi huku akiwataka viongozi kuhakikisha miradi yote inakamilika ndani ya wakati ili wananchi waanze kupata huduma.
Kwa upande wake Mkuu wa Hospitali ya Jeshi Lugalo Brig. Jenerali Agatha Katua amesema Hospitali ya Jeshi Lugalo ilipokea fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 4.4 ambapo mpaka sasa tayari wameshanunua mashine ya kufua hewa ya oksijeni kutoka Borahi Kuu ya Dawa, huku ujenzi wa jengo la kuwekea mashine hizo na kutoa huduma ukiwa unaendelea.
Brigedia Jenerali Agatha Katua amesema kuwa wanaendelea na ujenzi wa jengo la Radiolojia ambapo wataweka huduma zote za radiolojia sehemu hiyo kwa kuweka mashine za CT, Scan, MRI, X-Ray, Ultra Sound.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa jengo la radiolojia na jengo la kufua hewa ya oksijeni, Mkurugenzi Mtendaji wa SUMA JKT Kanali Petro Ngata, amesema ujenzi wa jengo la radiolojia umefikia asilima 62 huku wakitarajia kukamilisha ujenzi ifikapo Mwezi Septemba 2022 na Jengo la kufua hewa ya Oksijeni ujenzi umefikia asilimia 45 na wanatarajia kukamilisha ifikapo Mwezi Agosti 2022.