Serikali kupitia Mfuko wa Barabara (Road fund) imesema ipo tayari kupitisha kiasi cha shilingi Bilioni nne kwa ajili ya kumlipa mkandarasi atakayepatikana ili kuboresha miundombinu ya jangwani mara baada ya uhakiki wa makisio hayo kukamilika na kujiridhisha.

Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa Bodi ya mfuko huo, Mwenyekiti wa Bodi Joseph Haule, amesema kuwa nia ya serikali ni kuhakikisha  inatatua changamoto hiyo haraka kabla ya mvua za masika kuanza.

“Bodi imeona tatizo hili na tumeliona kama suala la dharura, ndio maana tumekuja hapa kujionea hali halisi ili kutafuta njia sahihi ya kutatua tatizo hili ambalo limekuwa kero kwa muda mrefu” amesema Haule.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Elius Mwakalinga, amesema kuwa serikali kupitia Wizara hiyo imeandaa mkakati wa muda mrefu kuhusu miundombinu hiyo, ambapo kwa sasa wataalamu wanafanya usanifu wa kina kwa ajili ya kuja na suluhisho la kudumu ikiwemo ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 300.

Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Dar es salaam, Mhandisi Julius Ngusa, ameeleza kuwa ofisi yake inaendelea kuhakikisha kuwa michanga inayotuama katika eneo hilo inatolewa kwa wakati ili kuruhusu magari kuweza kupita mara baada ya mvua kunyesha.

Hayo yamejiri waakati wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara walipotembelea eneo la Jangwani kujionea hali halisi ya miundombinu katika eneo hilo, ambayo imekuwa  ikiathiriwa na mvua na kusababisha kufunga mawasiliano ya watumiaji wa barabara ya Morogoro hususan eneo hilo kila mwaka.

Jengo la mama na mtoto Mwananyamala kuanza kazi
Imethibitishwaa Rihanna na A$AP Rocky kutoka kimapenzi