Chama cha Waagizaji na Wasambazaji Mafuta Tanzania – TAOMAC, kimesema bila upatikanaji wa dola kitashindwa kuagiza Mafuta, kauli ambayo wameitoa mara baada ya kukutana na Waziri wa Nishati, January Makamba jijini Dar es Salaam.

Katika kikao hicho cha Agosti 4, 2023 TAOMAC walitoa taarifa ya mwenendo wa biashara ya mafuta duniani na hapa nchini pamoja na kuwasilisha changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya mafuta hususani suala la upatikanaji wa dola za Marekani.

Makamu Mwenyekiti wa TAOMAC, Salim Baabde alisema, “biashara yetu inafanyika kwa kutumia Dola za Marekani na inapotokea dola inakuwa adimu sokoni inaathiri moja kwa moja bei ya uagizaji ambayo mwisho wa siku inaathiri bei ya mafuta kwa mtumiaji wa mwisho.”

Kwa upande wake Waziri Makamba amewashukuru kwa ushirikiano waliutoa kuhakikisha nchi inapata mafuta muda wote na kusema mlango wake uko wazi wakati wote kwa ajili ya mashauriano.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Kamishna wa Petroli na Mafuta Ndg. Michael Mjinja, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile na wataalamu kutoka Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja – PBPA.

Luis Enrique kuondoka Paris-Saint German
Jeshi lapanga mkakati kuingilia kati Sakata la Niger