Kamishina Mkuu wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR), Volker Türk amezindua ombi la dola milioni 452 ili kusaidia kufadhili kazi muhimu kwa mwaka 2023 na kuhuisha haki za binadamu duniani.
Akizundua ombi hilo mjini Geneva Uswisi, ikiwa ni mahsusi kwa ajili ya mfuko wa kujitolea kwa nchi wanachama na wahisani binafsi, Türk amesema bila haki za binadamu hakutakuwa na amani ya kudumu, hakuna maendeleo endelevu, wala haki.
Amesema, anatumai kwamba maadhimisho ya 75 ya azimio la kimataifa la haki za binadamu na katiba ya Umoja wa Mataifa vitachagiza ongezeko la ufadhili na kuisaidia ofisi yake kuimarisha uwezo wa kukidhi mahitaji na maombi ya nchi na wadau wengine.
Aidha amefafanua kuwa, “Nitatumia maadhimisho haya kusisitiza nia yetu ya kuhuisha maneno na vipengelele vya azimio hili. Tunasisitiza vitendo nyumbani na kimataifa ambavyo vitashughulikia mapengo ya usawa, kuimarisha ulinzi wa hifadhi ya jamii na kukomesha ubaguzi na migogoro, changamoto za mazingira nk.”