Jumla ya sh. Bilioni 166.24 ambazo ni sawa na wastani wa asilimia 22 za makisio ya mwaka, zimekusanywa nchini katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka ya Julai hadi Septemba 30, 2019 kufuatia malengo ya ukusanyaji Sh. Bilioni 765.48.

Hayo yamebainishwa jijini Dodoma hii leo Oktoba 21, 2019 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Seleman Jafo na kusema Mkoa wa Dar es salaam umeongoza kwa ukusanyaji wa mapato ghafi kwa sh. Bilioni 39.53.

Amesema Mkoa wa Kigoma umekuwa wa mwisho kwa makundi ya mikoa baada ya kukusanya Sh. Bilioni 2.12 na kwamba kwa wastani ipo mikoa ambayo imefanya vizuri na kuhamasisha watendaji kuendelea kufuata misingi ya kazi zao ili kuleta ufanisi kwenye ukusanyaji wa mapato.

“Mkoa wa Kigoma imeburuza mkia kwa makundi ya mapato ghafi na imekusanya bilioni 2.12 katika takwimu za kimapato kwa robo ya kwanza ya mwaka hadi kufikia tarehe 30 ya mwezi Septemba 2019 na hii ni kwa mujibu wa mlinganisho husika,” ameongeza Jafo

Aidha amefafanua kuwa kwa kulinganisha makundi  ya Halmashauri, miji, Manispaa na Majiji Wilaya ya Buhigwe iliyopo Mkoani Kigoma imekuwa ya mwisho kwa makundi yote baada ya kukusanya Sh. Milioni 35 na kudai kuwa juhudi za dhati zinahitajika ili kila eneo la ukusanyaji mapato liweze kufikia malengo.

Waziri huyo wa TAMISEMI amebainisha kuwa katika majiji Dar es salaam imeongoza kwa kuwa na asilimia 38 wakati Jiji la Dodoma likiwa na ailimia 18, huku Manispaa ya Sumbawanga ikiongoza kundi hilo kwa asilimia 42.

Zingine ni Manispaa ya Kigoma Ujiji iliyo na asilimia 9, huku kwa upande wa miji Tunduru ikiwa kinara kwa kuwa na asilimia 39, na mji wa Nanyamba ukiburuza mkia kwa kuwa na makusanyo ya asilimia 4 na kuwataka wakurugenzi ambao  maeneo yao hayajafanya vizuri kujitathmini.

“Kwahiyo jumla ya Sh. Bilioni 166.24 zimeshakusanywa na zipo halmashauri ambazo zimefanya vibaya na zipo ambazo zinastahili pongezi kwamakusanyo mazuri  sasa wakurugenzi ambao maeneo yao hayajafanya vizuri kwa ukusanyaji wa mapato wanatakiwa kujitathmini,” amesema Waziri  Jafo.

Aristica Cioaba arudi Azam FC, Ndayiragije atimkia Stars
Upelelezi kesi ya aliyemuua na kumchoma moto mke wake yakamilika