Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule, amesema kuwa Serikali imetenga jumla ya Shilingi Bilioni 18 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara tatu mkoani humo.
Ameyasema hayo wakati akifungua semina ya mafunzo kwa wadau wa usafirishaji kuhusu Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018 inayofanyika kwa siku moja mkoani humo.
“Katika Bajeti ya Serikali ya mwaka 2021/2022, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Ujenzi), kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), imetenga Shilingi Bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Nyamirembe hadi Katoke (Km 50), Bilioni 6 kwa ajili ya barabara ya Geita hadi Kahama (Km133), na Shilingi Bilioni 2 kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya Geita hadi Nzega (Km 54),” amesema Senyamule.
Ameongeza kuwa barabara hizo tatu ambazo hadi sasa zimetengewa jumla ya shilingi Bilioni 18, zinaendelea na taratibu za ujenzi, vilevile kwa barabara ya Katoro hadi Ushirombo ambayo iko kwenye mpango wa ujenzi inaendelea kufanyiwa usanifu na upembuzi yakinifu na inatarajia kupata fedha za ujenzi kutoka Benki ya Dunia.
Mkuu wa Mkoa huyo ameitaka TANROADS kuongeza wigo wa utoaji wa elimu kuhusu sheria ya uzibiti uzito wa magari ili kuondoa changamoto za uharibifu wa barabara unaofanywa na magari yaliyozidisha uzito kwani Serikali inatumia fedha nyingi katika ujenzi na ukarabati wa barabara nchini, fedha ambazo zinaweza kuelekezwa kwenye miradi mingine yenye uhitaji endapo ulinzi wa miundombinu ya barabara nchini utaimarishwa.
“Msukumo wa mafunzo haya unatokana na changamoto za mara kwa mara kwa baadhi ya wasafirishaji kutofahamu sababu zinazopelekea gari kukutwa limezidisha uzito katika mizani za TANROADS ambapo katika kituo kilichotangulia gari hilo hilo lilipimwa na halikuwa limezidisha uzito” amefafanua Senyamule.