Takriban watu bilioni 2.2 kote duniani, wanaishi na changamoto ya uoni hafifu au upofu na kufanya Shirika la afya duniani WHO, kutoa rai ya kuhakikisha fursa ya huduma za macho zilizo bora, jumuishi na kwa wote zinapatikana.

Kwa mujibu wa WHO, ambayo Oktoba 14, 2022 imeadhimisha siku ya uoni duniani, nchi za Kusini Msashariki mwa Asia ndizo zilizoathirika zaidi na matatizo ya uoni hafifu au upofu, zikibeba asilimia 30 ya watu bilioni 2.2 walio na matatizo ya uoni.

Imesema, inazitaka nchi hizo kuongeza juhudi ili kuhakikisha kila mtu anapata ufikiaji sawa wa huduma za afya ya macho za viwango na za kina, kulingana na mpango mpya wa utekelezaji wa kikanda wa mwaka 2022-2030 uliopitishwa kwa ajili ya huduma ya macho inayotoa kipaumbele kwa watu.

WHO imeongeza kuwa, angalau visa bilioni 1 vya ulemavu wa kuona vingeweza kuzuiwa au bado havijashughulikiwa na kusisitiza kwamba matatizo ya macho yanaathiri watu wa aina zote za maisha na kwamba Watoto wadogo, wazee, wanawake, watu wa vijijini na makundi ya walio wachache ndio walio katika hatarini zaidi.

Takwimu za shirika hilo la afya duniani, zinaonyesha kuwa mwaka 2020 makadirio ya hasara za kiuchumi zilizotokana na uoni hafifu au upofu zilifikia dola bilioni 411, huku idadi ya watu wenye matatizo ya kutoona karibu ikitarajiwa kuongezeka kutoka watu bilioni 1.8 mwaka 2015, hadi kufikia watu bilioni 2.1 ifikapo mwaka 2030.

Ili kusongesha haraka mchakato wa kukabiliana na changamoto hiyo ya macho, WHO imependekeza mambo matatu ya kuzingatia ya kujumuisha huduma za macho katika huduma zilizopo za afya, kuimarisha nguvukazi ya wahudumu wa afya ya macho na kuongeza fursa ya upatikanaji wa vifaa vya msaada, teknolojia mpya na kuchagiza utafiti.

Idadi ya vifo mlipuko mgodini yafikia 40
Kenya yakanusha madai kutolipa deni la China