Serikali imetenga bilioni 24.4 kwaajili ya kuwasaidia vijana waliotumia dawa za kulevya, na kuhakikisha vijana wanakuwa salama na kuokolewa kutoka kwenye uraibu wa matumizi ya dawa za kulevya.
Hayo yamesemwa na Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Bunge, Sera na Uratibu Jenista Mhagama ambapo amesema asilimia kubwa ya vijana ndiyo nguvu kazi ya Taifa katika kuleta maendeleo ndio maana serikali imeamua kuwekeza nguvu kubwa katika kuwasaidia vijana kuweza kujikwamua katika changamoto hiyo.
“Serikali inatumia gharama kubwa kutibu watumiaji wa dawa za kulevya na tayari mikakati ya kujenga kituo kikubwa cha kuwahudumia inaendelea,” amesema Mhagama.
Naye, Kamishna Jenerali Aretas Lyimo kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya(DCEA) amesema mpaka sasa wananchi 16 wamechukuliwa hatua kwa kujihusisha na ulimaji wa zao la bangi mkoani Arusha.
“Tumekuwa tukitoka elimu kwa wananchi juu ya madhara ya dawa za kulevya kwani zimekuwa zikileta athari kubwa kwenye ubongo wa binadamu na tunataka kuhakikisha zao hilo linaisha kabisa kwa jiji la Arusha na kwa watakaokaidi watachukuliwa hatua kali za kisheria “amesema Lymo.
Aidha ametoa wito kwa vijana waliotoka kwenye uraibu wa matumizi ya dawa za kulevya na kuacha biashara ya dawa za kulevya wana haki ya kuomba fedha katika mfuko wa halmashauri ili waweze kujiajiri pamoja na kuitaka jamii kuacha kuwanyanyapaa vijana wanaotumia dawa ya kulevya.
Kwa upande wa vijana waliotumia madawa ya kulevya wameiomba serikali pamoja na wadau kuweza kuboreshewa huduma kwa watumiaji wa dawa za kulevya huku wakisema wamekuwa waelimisha Rika kwa jamii na kuwa mabalozi kwa jamii.