Serikali imesema inatambua changamoto wanazokabiliana nazo wanafunzi wenye mahitaji maalum nchini kote na ndio maana inafanya jitihada za kuhakikisha inaweka mazingira rafiki ya kufundishia na kujifunza ili kila Mtanzania anufaike na fursa za elimu.
Hayo yamesemwa na Rais Samia Suluhu Hassan leo Machi 7 katika ziara yake maalum katika Shule ya Sekondari Benjamini Mkapa huku akianisha kuwa jitihada hizo zimelenga kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalum wanapata elimu bora.
Amesema baadhi ya jitihada hizo ni pamoja na Serikali imeendelea na mpango wake jumuishi wa 2021-2026 ambao utazingatia utoaji wa elimu jumuishi katika ngazi zote za elimu lengo likiwa ni kutoa elimu bora kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
“Tunafanya hivyo kwa sababu tunatekeleza azimio la kimataifa namba 4 katika maadhimio ya maendeleo endelevu yanayozungumzia elimu ikitutaka kutoa elimu yenye usawa kwa wote,” amesema.
Pia amesema kuwa Serikali imeandaa miongozo kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa elimu maalum na jumuishi nchini.
“Miongozo hiyo ni pamoja na ule wa usimamizi na uwendeshaji wa taasisi zinazotoa elimu maalum na jumuishi wa mwaka 2021 pamoja na ule wa ujenzi wa majengo ya serikali yanayozingatia wanafunzi wa mwaka 2020,”alisema.
amesema mbali na ujenzi wa madarasa, Serikali imeshatumia kiasi cha Sh5.9 bilioni kwa ajili ya ununuaji wa vifaa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Vilevile, ameshukuru uongozi wa mkoa, wilaya na shule ya sekondari ya Benjamini Mkapa kwa kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa na kueleza kuwa shughuli ile ilimpa furaha ya kuona anakumbukwa
“Siku ile nilikuwa nimejiandaa kwa mahojiano asubuhi na baadae jioni kukata keki na wanangu, lakini walimu wanafunzi na uongozi wa mkoa na Wilaya mkatayarisha shughuli kubwa ambayo sikuwa na taarifa nayo, hivyo ninashukuru sana,” amesema.