Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, chini ya Wakala wa Ufundi na umeme Tanzania TEMESA imetenga fedha kiasi Cha shillingi Bilioni 6.3 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kwaajili ya kuvifanyia ukarabati vivuko Nchini ambavyo vimefikiwa muda wake wa kukarabatiwa
Hayo yamesemwa leo wakati wa mapokezi ya Kivuko Cha MV Mafanikio kilichorejea kutoa huduma Mkoani Mtwara baada ya kukamilika kwa ukarabati wake uliochulua takriban miezi miwili na nusu
Akizunguma na wananchi waliofika kushuhudia tukio la upokeaji wa kivuko hicho lililofanyika katika eneo la Msemo Shangani Mjini Mtwara katika kivuko cha Msangamkuu – Msemo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti amesema ni utaratibu wa kawaida kwa Serikali kuvifanyia vivuko ukarabati kila inapopita miaka minne hadi mitano ili kuviwezesha kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle, amesema ukarabati wa kivuko cha MV. MAFANIKIO umefanywa na kampuni ya M/s Songoro Marine Transport Ltd. Boat Yard ya jijini Mwanza kwa gharama ya shillingi milioni 493.6
‘’Baadhi ya kazi zilizofanyika katika ukarabati huu ni pamoja na Kuweka deki mpya ya magari, kuweka milango mipya miwili (2-New ferry ramps), kuweka ramp lifting cylinder cover mpya, kutengeneza mifumo ya steering, propulsion pamoja na injini na kupaka rangi kivuko chote.’’ Amesema Mhandisi Maselle.
Aidha vivuko vitakavyokarabatiwa ni pamoja na MV. Kitunda (Lindi), MV Tanga (Pangani Tanga), MV Kazi na MV magogoni (Dar es salaam), MV Ruhuhu (Ruvuma) pamoja na vivuko vinavyofanya kazi kwenye ziwa Victoria ambapo amesema serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 6.3 kwa ajili ya ukarabati wa vivuko hivyo.
Kivuko cha MV. MAFANIKIO kina uwezo wa kubeba abiria 100 na magari sita sawa na tani 50 na kinatoa huduma kati ya Msangamkuu na Msemo Mkoani Mtwara.