Serikali imetenga kiasi cha takribani Shilingi Bilioni 8.59 kwa ajili ya kuvifikishia umeme vitongoji ambavyo havina umeme katika Mkoa wa Kilimanjaro, katika fedha hizo Wilaya ya Same imetengewa zaidi ya Shilingi Bilioni 3.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameyasema hayo wakati akizindua Mradi wa Ujazilizi Umeme Vijijini Fungu la Pili A ngazi ya Mkoa uliofanyika katika kijiji cha Mheza wilaya ya Same Mkoa wa Kilimanjaro, utakaotekelezwa kwa muda wa miezi 12.
Aidha, amewakumbusha viongozi wa Serikali za Mitaa katika ngazi ya Kata na Vijiji kutenga maeneo maalum ya uwekezaji wa Viwanda ili yaweze kupelekewa miundombinu ya umeme wakati wa utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini.
“Tumieni umeme kufanya biashara muongeze thamani ya mazao ya kilimo na mifugo kwa kuanzisha viwanda” Amesema Waziri Kalemani.
Katika hatua nyingine Waziri Kalemani amewaagiza wakandarasi wanaojenga miundombinu ya kusambaza umeme vijijini kupeleka umeme katika maeoneo maalum ambayo yametengwa kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki, Anne Kilango Malecela, ameishukuru Serikali kwa kupelekewa miradi hiyo ya kusambaza umeme vijijini na kuomba maeneo ambayo bado hayajafikishiwa umeme yapatiwe nishati hiyo.