Wakala wa Nishati Vijijini – REA, imewekeza kiasi cha shilingi 80 bilioni 80 zitakazotekeleza miradi mbalimbali ya usambazaji wa umeme vijijini Mkoani Kagera wenye jumla ya vijiji 662, huku Vijiji 512 sawa na asilimia 77.3 vikipata umeme kupitia miradi ya awali.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy wakati Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko alipokuwa akiwasha umeme Kijiji cha Mubaba na cha Nyantakara vya Wilayani Biharamulo, mkoani Kagera.
Amesema, “kupitia Wakala wa Nishati Vijijini ndani ya Mkoa wa Kagera imewekeza shilingi bilioni 80 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kusambaza umeme vijijini, na hivi ninavyoongea ndani ya mkoa huu kuna miradi mitano inatekelezwa.”
Aidha, ametaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na mradi wa REA awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, mradi wa kupeleka umeme pembezoni mwa miji, mradi wa ujazilizi, mradi wa kupeleka umeme kwenye migodi midogo na maeneo ya kilimo na mradi wa kupeleka umeme kwenye Vituo vya Afya na Pampu za Maji.