Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura) wamepanga kutumia takribani Sh. bilioni 800 kufanikisha ukarabati wa zaidi ya kilometa 400 za barabarani nchini.

Akizungumza na wadau wa barabara Mkoa wa Geita ,Mhandisi wa Miradi kutoka Tarura, Raymond Kileo ambaye pia ni mratibu msaidizi wa mradi wa RISE,amesema kuwa Ukarabati huo unafanyika kupitia mradi Shirikishi wa Maendeleo ya Barabara na Utumiaji wa Fursa za Kijamii na Kiuchumi (RISE) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa ushirikiano na serikali.

Kileo amesema kati ya fedha hizo, takribani Sh bilioni 692 zimetolewa na Benki ya Dunia huku takribaniSh bilioni 115 zikiwa zimetolewa na serikali ya Tanzania, mradi huo utatekelezwa kwa kushirikisha makundi mbalimbali ya kijamii ikiwamo wenye ulemavu, wazee,wanawake na watoto ili kutoa vipaumbele kwenye maeneo yenye uhitaji zaidi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe, Elias Kayandabila amesema mradi wa RISE umekuja wakati muafaka kwani hadi sasa barabara nyingi kwenye halmashauri yake hazina kiwango cha lami jambo ambalo limekuwa kikwazo kwa shughuli za usafirishaji wakati wa mvua.

Kayandabila amesema ujenzi wa barabara kwenye halmashauri hiyo utachagiza maendeleo ya kiuchumi hasa kupitia shughuli za kilimo kutokana na ukweli kwamba asilimia kubwa ya wakazi ni wakulima hivyo wataweza kusafirisha mazao yao kwa urahisi hadi kuwafikishia wateja sokoni ama nje ya wilaya.

‘Ninamtafuta Lowasa’
Sigara ilivyo hatari kwa mama mjamzito