Ili kumng’oa Kiungo Mshambuliaji ‘WINGA’ Vinicius Jr katika timu ya Real Madrid, klabu inayomtaka itapaswa kulipa dau la euro bilioni moja, ambazo ni zaidi ya Sh. Trilioni 2.6 za Tanzania.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mbrazili huyo kumwaga wino kwenye mkataba mpya wa miaka minne ili kuendelea kukipiga Real Madrid ya Hispania.
Tovuti ya 90mins imeripoti kuwa, katika mkataba huo kuna kipengele kinachoweza kumruhusu nyota huyo kutimka Real Madrid kwa euro bilioni moja.
Vinicius Jr alimwaga wino katika mkataba huo mwanzoni mwa juma hili, kuendelea kusalia kwa mabingwa hao mara 14 wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, hadi mwaka 2027.
Winga huyo mwenye umri wa miaka 23, amefikia hatua hiyo baada ya majadiliano ya pande zote mbili kwa miezi kadhaa.
Vinicius alijiunga katika kikosi cha Real Madrid mwaka 2018, akitokea katika klabu ya Flamengo ya nchini Brazil.
Imeripotiwa kuwa, Vinicius Jr na uongozi wa Real Madrid walifikia muafaka wa dili hilo mapema mwaka huu, kabla ya mwanzoni mwa mwezi huu kukamilisha baadhi ya vipengele na kisha kutia saini.
Mkataba huo umemfanya Vinicius Jr kuwa miongoni mwa nyota wanaolipwa fedha nyingi katika klabu hiyo kutoka jiji la Madrid.
Ufundi wa kusakata soka, kasi na kufunga mabao kumemwezesha nyota huyo kuwa mmoja kati ya wachezaji bora duniani kwa miaka michache iliyopita.
Katika mashindano yote msimu uliopita, Mbrazili huyo alifungia Real Madrid mabao 23.
Katika Ligi Kuu ya Hispania msimu huu, nyota huyo amefunga mabao mawili na kutoa pasi moja ya bao katika michezo minane aliyocheza.