Wakulima wa mazao aina mbili ya mpunga na mahindi nchini kuanza kunufaika na bima mazao kutokana na kukabiliwa na hasara kubwa pindi zinapotokea changamoto katika uzalishaji wa mazao hayo.
Miongoni mwa mikoa inayoanza kunufaika na bima ya mazao hayo hapa nchini ni pamoja mikoa ya Ruvuma kwa upande wa halmashauri ya wilaya ya Songea na Madaba, mkoa wa Njombe kwa upande halmashauri ya wilaya ya Njombe na Ludewa pamoja na Mkoa wa Morogoro kwa upande wa halmashauri ya Kilombero na Mvomero kutokana na kupatikana kwa wakulima wengi katika maeneo hayo.
Akizungumza na Dar24 baada ya uzinduzi wa bima hiyo uliofanyika katika kijiji cha Mtwango kilichopo wilayani Njombe, Joshua Ongaga meneja mradi wa bima ya mazao (WEKU) amesema bima hiyo itaanza kupatikana katika mikoa hiyo kwa wasambazaji wote wa pembejeo pamoja na vyama vya wakulima kwa kuanza na wakulima wadogo wanaolima shamba lenye ukubwa wa nusu ekari au chini ya ekari moja.
“Tofauti na aina zingine za bima ya mazao, bima ya kilimo ya lima salama, wakulima wataweza kuinunua moja kwa moja kutoka katika vyama vyao katika mfumo wa kadi scratch cards, hivyo wakulima wana uwezo wa kutumia simu zao za mkononi kwa kusajili bima zao huku kadi moja ya bima ikiuzwa kwa gharama ta Tsh 5,000 na ikilinda ghalama ya uzalishaji yenye thamani ya Tsh 70,000 tu, tunatarajia wakulima wawekeze kwa uhakika kwamba mkulima akiingia shambani awe na uhakika wa matokeo wa yale aliyoyawekeza”amesema Ongaga
Consolatha Gabone ni meneja mamlaka ya usimamizi wa bima nyanda za juu kusini, anasema bima ya kilimo kwa sasa ni muhimu kwa kuwa serikali kwa sasa inahamasisha kilimo cha biashara hivyo ni lazima wakulima kuwa na bima kutokana na changamoto zilizopo katika kilimo.
“Bima ya mkulima ni kitu muhimu sana na serikali yetu sasa hivi inataka kilimo cha biashara kinachoweza kumkwamua mkulima, haiwezekani kufikia ndoto bila ya kuwa na bima kwasababu kilimo kina changamoto kubwa sana kama hali ya hewa, wadudu, kukosa soko hivyo kuna mambo mengi yanaokinga ndoto ya mkulima kufikiwa”amesema Gabone
Afisa kilimo wa mkoa wa Njombe Wilson Joel amewaasa wakulima wa mkoa wa Njombe kuipata elimu vizuri juu ya bima kutoka kwa wataalamu waliopo ili kuondoa changamoto wanazoweza kukutana nazo wakati wa matumizi ya bima.
Naye afisa kilimo kutoka mkoa wa Ruvuma Adrew Tarimo amewataka wanaume kutumia pesa katika bima badala ya kucheza michezo ya kubahatisha huku afisa kilimo kutoka mkoa wa Morogoro Peter Gama akiwaomba wakulima kuwatumia vizuri wataalamu wa kilimo katika changamoto zozote.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Njombe aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Jeritha Mligo ambaye ni afisa kilimo wilaya hiyo alisema zipo changamoto nyingi ikiwemo ukame na mvua za mawe zinazotokea bila taarifa hivyo ni wajibu kwa wakulima kuchangamkia fursa hiyo.
Karibia asilimia 65%-70% ya watanzania wanaishi vijijini na wengi wao wanajishughulisha moja kwa moja na shughuli za kilimo cha mazao mbali mbali, Shughuli hizo za kilimo zinachangia karibia asilimia 32% ya pato la Taifa kutokana na biashara ya mazao ndani na nje ya nchi.
Mabadiliko ya hali ya hewa,kuongezeka kwa wagonjwa ya mimea na wadudu, ni baadhi matatizo yanayowakabili wakulima wengi nchini, Matatizo haya yamepelekea wakulima wengi kuacha kujishughurisha na shughuri zingine zisizohisana na kilimo.
Hivyo kampuni ya bima ya Reliance,kwa kushirikiana na na kampuni ya ACRE Africa wataalamu wa kutengeneza bima za mazao Africa, wameanzisha bima hiyo ya mazao kwa wakulima wa mahindi na mpunga Tanzania. Bima hii ya mazao itaanza kupatikana kwa wakulima wa kanda ya kusini katika mikoa ya Njombe,Ruvuma na Morogoro kuanzia msimu wa kilimo wa mwaka 2019/2020.
Lakini ili kuhakikisha wakulima wananufaika na huduma hiyo ya bima, kampuni ya Reliance inashirikiana na taasisi za Alliance for Green Revolution in Africa (AGRA) na Tanzania Association of Professional business Development (TAPDBS) kuhakikisha wakulima wanapata mafunzo ya kutosha kuhusu kilimo bora ili waweze kulima kilimo cha kisasa.