Bingwa wa michuano ya Wasichana chini ya umri miaka 18, inayoandaliwa na Baraza la Vyama Vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), anatarajiwa kupatikana leo.
Bingwa huyo atapatikana katika mechi kati ya Tanzania na Uganda, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya jijini la Dar es Salaam.
Kabla ya mchezo huo utakaoanza saa 12:00 jioni, kutakuwa na mechi nyingine ya kati ya Zanzibar dhidi ya Burundi utakaopigwa saa 9:00 alasiri.
Tanzania na Uganda zinashuka dimbani huku kila mmoja akihitaji alama tatu pekee kutwaa ubingwa wa mashindano hayo baada ya kushinda michezo yote mitatu iliyopita.
Katika msimamo wa mashindano hayo, Uganda inaongoza ikiwa na alama tisa sawa na Tanzania ambapo zikitofautiana idadi ya mabao ya kufunga.
Uganda inaongoza kwa mabao mengi ya kufunga ikifikisha 11 na Tanzania ina mabao sita.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Bakari Shime, alisema utakuwa mchezo mgumu na wenye ushindani mkubwa, sababu timu zote zina alama sawa na kila mmoja anahitaji ushindi katika mechi ya mwisho.
“Mechi ni ngumu kwa sababu ya upinzani wetu, lakini hatuhitaji kuona kombe linaondoka hapa kwetu, tutapambana kuhakikisha tunapata ushindi katika mchezo huo na kutwaa ubingwa wa CECAFA U-18,” alisema.
Aliongeza kuwa ana imani na wachezaji wake watafanya vizuri baada ya kufanyia kazi mapungufu ya michezo iliyopita.
Tanzania ilianza mashindano hayo kwa kuwafunga Burundi mabao 3-0, kisha wakaitungua Ethiopia mabao 2-0 na kuwapiga bao 1-0 Zanzibar.
Wakati Uganda wao walianza kwa kuwaadhibu Ethiopia bao 1-0, wakawanyuka Zanzibar mabao 3-0 na kuwafunga Burundi mabao 7-0.
Tanzania na Uganda zipo katika bingwa wa kampeni za kusaka mashindano hayo ambayo yanafanyika kwa mara ya kwanza lakini Ethiopia wamejihakikishia nafasi ya tatu huku Zanzibar na Burundi wakitafuta nani atashika nafasi ya nne na ya tano.