Baba wa binti aliyezama kwenye bwawa la kuogelea huko Canada wakati akijirekodi moja kwa moja kwenye mtandao wa Facebook, amezungumzia tukio la kumpoteza binti huyo.
Nyabuto John Kiyondi mwenye Umri wa miaka 56, amesema aliiona video ikisambaa mitandaoni na ilimsikitisha zaidi kwa kuwa haikuwa nzuri.
“Nililia sana, Aliwasiliana na mimi siku 2 kabla ya tukio hilo kutokea na alikua akionekana yupo sawa na ana furaha, hakuwa na tatizo lolote na aliniahidi kunitumia simu,” Nyabuto alisema.
Aliongeza kuwa, “Wendy aliishi Canada na kaka yake ambaye ni mmoja kati ya ndugu zake watano, huku akisomea fani ya unesi na alikuwa akijitolea kama muhudumu wa afya na yeye ndiye alikuwa mhudumiaji mkuu wa familia hapa Kenya sasa tunarudi hatua ya mwanzo kabisa kiuchumi,”
Baba huyo ambaye ni Mkulima akiishi Kisii, Kusini Magharibi mwa Kenya, amesema, “Wendy alikua akimsaidia kuhudumia ada za wadogo zake ambao bado wapo kwenye elimu za chini, na gharama nyingine za Maisha ya nyumbani, na sasa sina uhakika tena wa maisha yataendaje kwa sababu mimi pekeyangu siwezi,”
Nyabuto ameomba wachangiaji wamsaidie ili mwili wa mtoto wake urudi Nchini Kenya kwa sababu mila na tamaduni zao zinawataka mtu azikwe aneo alilozaliwa.
“Kutokana na Mila na desturi zetu mtu anatakiwa azikwe mahali alipozaliwa, sitajiskia vizuri endapo sitaweza kumzika mwanangu.”
Kwa hesaba za haraka ni kuwa ili kuweza kuusafirisha mwili wa Wendy mpaka Kenya kutoka Canada, itawalazimu kama familia kuuza kila kitu cha thamani, Kaka yake aliyekuwa anaishi naye, Enock, amesema mpaka sasa wameshaanza kukusanya pesa kupitia Kampeni ya ‘GoFundMe’ kiasi cha Dola elfu 38 ambayo ni takriban shillingi Milioni 88 za kitanzania ili kuweza kumzika Wendy.
Hellen Wendy Nyabuto alikuwa na miaka 23, alionekana akihangaika kujikwamua baada ya kuzama akiwa anajipiga picha wakati anaogelea akiwa moja kwa moja anaongea wa wafuasi wake kwenye mtandao wa Facebook.
Mwili wake ulipatikana masaa machache baadae chini ya bwawa hilo huko Collingwood, Ontario ambapo alikua akifanyia kazi.