Waswahili wanasema ‘utu uzima dawa’. Ndicho kilichoonekana Jumamosi iliyopita kwenye jukwaa lililovuta usikivu wa dunia ya muziki, pale ‘baba’ alipoamua kumuomba radhi mwanaye hadharani ili amani iendelee.
Birdman, alipanda kwenye jukwaa la tamasha la Lil Wayne (Lil Weezyana) lililofanyika New Orleans na kutangaza mbele ya maelfu waliohudhuria kuwa anaomba radhi kwa rapa huyo kwa yote yaliyowahi kutokea na kusababisha msuguano kati yao.
Birdman alisema kuwa alijua wakati wote kuwa siku kama hiyo ingekuja kutokea na kwamba anashukuru imetokea huku akimuita Lil Wayne kuwa ni rapa bora zaidi duniani.
“Nilijua siku kama hii itakuja kutokea, lakini sikujua ni lini. Lakini huyu mshikaji wangu hapa, rapa bora zaidi. Rapa mkali zaidi… na ninataka kumuomba radhi huyu mshkaji wangu mbele ya dunia nzima,” alisema Birdman kwa tafsiri isiyo rasmi iliyoondoa maneno yenye ukakasi.
Alisisitiza kuwa YMCMB ambayo ni muunganiko wa lebo yake kubwa inayommiliki Lil Wayne na ile ya Lil Wayne (Young Money) hazitatengana hadi kifo.
Wawili hao baada ya hapo walikumbatiana na baadaye kazi ikaendelea huku shangwe likifunika kila kona.
Tukio hilo limekata mzizi wa fitna kufuatia bifu iliyokuwa kati yao. Wayne aliwahi kufungua mashtaka dhidi ya Birdman na Cash Money akidai kulipwa $51 milioni mwaka 2015, akitaka mkataba kati yake na lebo hiyo uvunjwe. Ilidaiwa kuwa wawili hao walifikia muafaka Juni mwaka huu bila kuweka wazi nini hasa walichoafikiana hadi kuachana na kesi hiyo.
Hali hiyo inatoa matumaini zaidi kuwa albam ya Lil Wayne ya Carter V, ambayo alikuwa anailalamikia lebo hiyo kwa kuichelewesha itatoka kabla mwaka huu kuisha.
“Albam itatoka mwaka huu. Nawahakikishia mtaipata mwaka huu,” Birdman aliwahi kukaririwa Februari mwaka huu. Ahadi hii sasa inaonesha kila dalili ya kutekelezwa.