Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’ Joseph “Sepp” Blatter amekumbana na adhabu nyingine ya kifungo, kufuatia madudu aliyowahi kuyafanya wakati wa utawala wake.
Blatter ambaye alianza kuliongoza shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’ kuanzia mwaka 1998 hadi 2015, amepewa adhabu mpya ya kifungo cha miaka sita itakayoanza kufanya kazi baada ya adhabu ya sasa itakapomalizika.
Adhabu ya awali ya kufungiwa kujihusisha na soka kwa mzee huyo mwenye umri wa miaka 85, inahusisha miaka minane ambayo ilitolewa baada ya kubainika alikua anatumia hivyo madaraka aliyokuwa nayo kwa kipindi cha miaka 17 ya utawala wake.
Blatter anatuhumiwa kutumia vibaya madaraka yake kwa kuidhinisha kiasi cha Dola 140 milioni (Sh 320 bilioni) kwa ajili ya kurekebisha Makumbusho ya FIFA, kiasi ambacho ni zaidi ya gharama halisi za ukarabati huo.
Kosa la sasa kwa Blatter pia linamuhusisha aliyekuwa katibu mkuu wa FIFA, Jerome Valcke ambapo kwa pamoja wanatuhumiwa kupokea zawadi ambazo zimetafsiriwa kama rushwa lakini pia matumizi mabaya ya ofisi pindi alipokuwa Rais.