Promota Bob Arum wa pambano wa bondia wa Uingereza Amir Khan na bingwa wa uzani wa Welterweight Manny Pacquiao ametoa taarifa za kulifuta pambano hilo pasi na kutoa sababu za kina.
Pambano la wababe hao wawili lilitangazwa kufanyika Aprili 28 mwaka huu, kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter mwishoni wa mwezi Februari, na lilipangwa kufanyikia huko Falme za Kiarabu (UAE). Mabondia hao wote walithibitisha kuwepo kwa pambano hilo kupitia mitandao yao ya kijamii.
Arum alitangaza kulifuta pambano hilo kupitia kituo cha televisheni cha ESPN cha nchini Marekani akiwaacha watu na maswali mengi pasi na majibu kutoka kwake kuhusu sababu za msingi.
”Ninazungumzia kuhusu pendekezo jingine lakini sio Khan. Khan hatakua mpinzani wa Manny,” Arum alisema kwa ufupi.
Pambano hilo la mwezi Aprili lilipangwa baada ya mashabiki wa Paqcuiao katika mtandao wa Twitter kumpigia kura Amir Khan kuwa mpinzani ambaye wangependelea bondia huyo mwenye umri wa miaka 38 kupigana nae.
Katika kura zilizopigwa na mashabiki wa Pacquiao kumpata mpinzani wake, Khan mwenye umri wa miaka 30 aliyeshinda medali ya fedha katika uzani wa Lightweight kwenye michuano ya Olimpiki mwaka 2004, alimshinda Kell Brook, raia wa Australia Jeff Horn na Mmarekani Terence Crawford kwa asilimia 48 ya kura hizo zilizopigwa na mashabiki wa Pacquiao.