Mwanamuziki na Mbunge maarufu nchini Uganda, Robert ‘Bobi Wine’ Kyagulanyi jana alikamatwa tena akiwa anajaribu kuondoka nchini humo kuelekea ughaibuni kwa ajili ya matibabu.
Kwa mujibu wa mwanasheria wake, mbunge huyo alikamatwa jana akiwa uwanja wa ndege licha ya kuwa Mahakama ilimpa dhamana na kuamuru arejeshewe hati yake ya kusafiria.
Imeelezwa kuwa Bobi Wine aliyekuwa ameshikiliwa jeshi la nchi hiyo kwa muda kabla ya kufikishwa mbele ya mahakama ya kijeshi akishtakiwa kwa uhaini, alibebwa na gari la polisi na kwamba mwanasheria wake hawajui kituo walichompeleka tena.
“Alikamatwa Alhamisi akiwa Uwanja wa Ndege, ingawa jaji aliatoa amri kuwa apewe hati yake ya kusafiria kwa sababu alitaka kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu,” BBC inamkariri Robert Amsterdam.
“Alitupwa kwa vurugu ndani ya gari la polisi. Mwanasheria wake hafahamu wamempeleka wapi na watu wake wa karibu wako kwenye taharuki,” aliongeza.
Mbunge huyo alikuwa akishikiliwa na kikosi maalum cha ulinzi wa rais na inadaiwa kuwa alipata maumivu makali kutokana na kipigo.
Kikosi hicho kilimshikilia Bobi Wine pamoja na wabunge wengine wa upinzani kutokana na kile kilichoelezwa kuwa alishiriki katika vurugu za uchaguzi mdogo ambapo gari la msafara wa Rais lilishambuliwa kwa mawe.
Bobi alifunguliwa mashtaka ya uhaini pamoja na kukutwa na silaha za moto alizodaiwa kuzimiliki kinyume cha sheria. Hivi sasa anashtakiwa kwenye mahakama ya kiraia.