Mbunge wa Uganda, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine jana alikutana na mjumbe wa bunge la Congress la Marekani, Bradley Sherman katika hatua ya kushawishi taifa hilo tajiri duniani kusitisha misaada kwa jeshi la Uganda.

Bobi Wine ambaye anadai kupigwa na vikosi vya jeshi la Uganda kwa kile kilichoelezwa kuwa alihusika katika vurugu zilizosababisha gari la msafara wa Rais Yoweri Museveni kushambuliwa kwa mawe, ameenda Marekani kwa ajili ya matibabu lakini ameanzisha pia harakati nyingine.

Mwanasiasa huyo anaonekana kuanza kuishawishi Marekani kuangazia suala la haki za binadamu pamoja na vipigo kwa wanasiasa wa vyama vya upinzani nchini Uganda.

“Katika kikao chetu, tuliainisha umuhimu wa mchakato wa demokrasia pamoja na wale wote ambao wameendelea kuumizwa kutokana na ukandamizaji wa kisiasa ndani ya Uganda,” Sherman alitweet, akiweka picha inayomuonesha akiwa na Bobi Wine na mkewe.

Timu ya Bobi Wine inaendelea kutafuta namna ya kuzungumza na Bunge la Marekani kuishawishi Serikali inayoongozwa na Donald Trump kusitisha msaada wa kijeshi kwa Serikali ya Uganda.

“Tunataka walipa kodi wa Marekani wafahamu kuwa pesa zao zinafadhili uonevu huu. Silaha za kijeshi tunazowapa Uganda zinatumika kuanzisha vita dhidi ya wananchi wa Uganda,” mwanasheria Robert Amsterdam aliwaambia waandishi wa habari jijini Washington, Alhamisi wiki hii.

Katika mkutano huo, Bobi Wine aliwaonesha waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya kimataifa majeraha aliyoyapata kutokana na kile alichodai ni kuwa ni kipigo na kuteswa akiwa mikononi mwa vikosi vya jeshi.

JPM atoa siri ya kumtoa bosi Takukuru, Lissu atoboa siri ya dereva wake
"Kwanini mnagombana wewe DC na RC? ningewatumbua leo leo- JPM