Mbunge ambaye pia ni mwanamuziki nchini Uganda, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine hajulikani alipo saa chache baada ya kutokea vurugu kubwa Jumatatu katika kampeni ya uchaguzi mdogo wa ubunge wa jimbo la Arua.
Jeshi la Polisi limethibitisha Jumanne asubuhi kuwa Bobi Wine sio miongoni mwa watu waliokuwa wanashikiliwa na jeshi hilo kwa kosa la kushambulia gari linaloongoza msafara wa Rais Yoweri Museveni.
Bobi Wine alionekana kwa mara ya mwisho kwenye mtandao wa Twitter Jumatatu jioni alipoandika kuhusu tukio la dereva wake kuuawa kwa kupigwa risasi kufuatia vurugu kati ya wafuasi wanaomuunga mkono mgombea wa upinzani na kikosi maalum cha ulinzi wa Rais kinachofahamika kama SFC.
Polisi walithibitisha kifo cha dereva huyo na kueleza kuwa risasi iliyompiga haikuwa imekusudiwa kumlenga.
Rais Museveni alikuwa katika eneo la Arua akimpigia kampeni mgombea wa chama tawala, Nusura Tipera wakati Bobi Wine alikuwa pia katika eneo hilo akimpigia debe Wandri ambaye ni mgombea binafsi.
Msemaji wa jeshi la polisi la Uganda, Emilia Kayima alieleza kuwa kabla ya kufika eneo la kampeni, msafara wa Rais Museveni ulikutana na gari aina ya tingatinga ambalo lilikuwa na riboni nyekundu likizuia msafara, lakini pia baada ya kumaliza kampeni moja ya gari lake liishambuliwa na wafuasi wa vyama vya upinzani.
Rangi nyekundu hutumiwa na vyama vya upinzani nchini humo na hutumiwa pia na Bobi Wine pamoja na Wandri ambaye ni mgombea binafsi.
Wapiga kura wa Arua wanatarajia kupiga krua Jumatano ya Agosti 15 mwaka huu kumpata mbunge.