Mbunge wa Uganda, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, amesema kuwa amejiandaa kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Bobi Wine ambaye ni mwimbaji maarufu nchini humo, ameweka wazi mpango huo kupitia mahojiano aliyofanya wiki hii na kituo cha runinga cha CNN akiwa nchini Marekani.
Mwanasiasa huyo ameeleza kuwa anaamini njia sahihi zaidi ya kubadili mfumo wa maisha ya watu nchini humo ni kuhakikisha wananchi wanauondoa madarakani utawala wa Rais Yoweri Museveni kupitia sanduku la kura.
“Tumekuwa tukijadili na timu yangu kuhusu hili, na sisi tumeamua kwa dhati kuwa nitapambana na Rais Museveni kwenye uchaguzi ujao wa urais,” amesema Bobi Wine.
Uganda ilifanya uchaguzi mkuu mwaka 2016 ambapo Rais Museveni alishinda na kupata ridhaa ya kuendelea kuiongoza nchi hiyo ya Afrika Mashariki, akimuacha mbali mshindani wake, Kizza Besigye.
Bunge la nchi hiyo limeondoa ukomo wa umri wa urais na kuongeza kipindi cha muhula wa urais na bunge kutoka miaka mitano hadi saba, hivyo nchi hiyo inatarajia kufanya uchaguzi mwingine mwaka 2023 badala ya 2021.