Mgombea urais nchini Uganda kutokea chama cha upinzani cha National Unity Platform (NUP) Robert Kyagulanyi Ssentamu maarufu Bobi Wine anatarajia kuendelea na shughuli zake za kampeni kesho Jumatatu Novemba 23, 2020 baada ya kampeni zake kukatizwa siku y Jumatano.

Katika ujumbe aliouweka hii leo kwenye mtandao wa Twitter, Bobi Wine ameashiria kutokata tamaa ya kile anachotaka kufikia.

Kwa mujibu wa msemaji wa chama chake cha NUP Joel Ssenyonyi, Bobi Wine atarejea katika kampeni zake kesho Jumatatu katika eneo la Kyenjojo na Fort portal na inasemekana kwamba kuna mipango ya kupanga tena kampeni katika maeneo alikotakiwa kufika kabla ya kukamatwa. 

Baada ya kuachiwa huru, Bobi Wine alisema wafuasi wake wamejitolea kuendelea kupigania mabadiliko nchini humo na kuongeza kuwa hatua ya kuongezwa kwa maafisa wa usalama ni ishara ya uoga, hofu na ukosefu wa matumiani.

Mapema Leo Jumapili, Bobi Wine alifanya maombi maalum na kutuma rambi rambi zake kwa familia zilizopoteza wapendwa wao wakati wa vurugu zilizotokea wiki hii baada ya kukamatwa kwake.

Kwa mujibu wa polisi nchini humo, idadi ya watu waliofariki katika maandamo yaliyofanyika siku ya Jumatano na Alhamisi imefikia watu 28, japo vyombo vya habari nchini Uganda vinanukuu vyanzo vya hospitali kuu kwamba idadi ya waliofariki ni watu 37.

Bobi Wine alikamatwa siku ya Jumatano alipokuwa akifanya mkutano wake wa kampeni katika eneo la Luuka na kupelekwa kituo cha polisi cha Nalufenya na aliachiwa kwa dhamana siku ya Ijumaa, baada ya kushtakiwa kwa kukiuka kanuni za kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona.

Iwapo atapatiakana na hatia, Bobi wine atakabiliwa na kifungo cha hadi miaka saba gerezani.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Novemba 23, 2020
Mahakama Pennsylvania yatupilia mbali madai ya Trump