Hatimaye Nahodha na Mshambuliaji wa Mabingwa wa Tanzania Bara mara nne mfululizo Simba SC John Raphael Bocco, ameibuka kinara wa ufungaji bora wa Ligi Kuu msimu wa 2020-21.
Bocco amemaliza msimu, huku akifunga mabao 16 ambayo yanamuweka kileleni mwa orodha ya wafungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mshambuliaji huyo mzawa amefunga bao lake la 16 leo Jumapili (Julai 18), dhidi ya Namungo FC waliokubali kichapo cha mabao 4-0.
Bocco amefunga bao la nne kwa mkwaju wa penati, akitanguliwa na Mshambuliaji kutoka DR Congo Chriss Mugalu aliyefunga mabao mawili na Meddie Kagere aliyefunga bao la kwanza dhidi ya Namungo FC.
Kwa mantiki hiyo Bocco anavunja utawala wa Meddie Kagere alietawala kwa misimu miwili mfululizo kama mfungaji bora wa Ligi Kuu 2018-19 na 2019-20.
Wanaomfuatia Bocco kwenye orodha ya ufungaji Bora ni Chriss Mugalu (Simba SC) mwenye mabao 15, Prince Dube (Azam FC) mwenye mabao 14 na Meddie Kagere (Simba SC) mwenye mabao 13.