Mshambuliaji wa klabu ya Simba SC John Bocco amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Novemba wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2020/21, huku kocha wa Ruvu Shooting Charles Boniface Mkwasa akichaguliwa kuwa kocha bora wa mwezi huo.
Bocco na Mkwasa wametwaa tuzo hizo baada ya kuwashinda wenzao waliongia nao fainali kwa mwezi Novemba katika uchambuzi uliofanywa juma hili na kamati ya tuzo za VPL, kutokana na mapendekezo ya makocha waliopo vituo mbalimbali ambavyo ligi hiyo inachezwa.
Bocco aliwashinda washambuliaji wawili alioingia nao fainali ambao ni Abdul-Rahman Mussa (Ruvu Shooting) na Deus Kaseka ( Young Africans).
Kwa upande wa kocha Mkwasa aliwashinda Mecki Mexime (Kagera Sugar) na Flugence Novatus (Gwambina FC), ambapo kocha huyo wa Ruvu Shooting aliiongoza timu yake kutoka nafasi ya kumi hadi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu, huku akishinda michezo mitatu na kutoka sare michezo miwili, ikiwa ndio timu iliyopata alama nyingi kwa mwezi Novemba.
Wachezaji wengine ambao tayari wameshatwaa tuzo hiyo ya mwezi kwa msimu huu ni Prince Dube wa Azam FC (Septemba) na Mukoko Tonombe wa Young Africans (Oktoba).
Makocha waliotwaa tuzo hiyo ni Aristica Cioaba aliekua Azam FC (Septemba) na Cedrick Kaze wa Young Africans (Oktoba).
TFF imekua na utaratibu wa kutoa tuzo ya mchezaji bora na kocha bora wa VPL kila mwezi, ambapo pia mwisho wa msimu kunakua na tuzo za wachezaji mbalimbali waliofanya vizuri, kwa msimu mzima ikiwemo tuzo ya mchezaj bora wa Tanzania.