Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), imetaka ndani ya siku 30 Taasisi na asasi 743 zijieleze kwa nini bodi za wadhamini wa taasisi hizo zisifutwe kutokana na kutotekeleza maelekezo ya kufanya marejeo ya katiba na kupeleka marejesho ya kila mwaka kwa mujibu wa sheria.
Taarifa ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Rita, Angela Anatory imeeleza kuwa wakala umefikia hatua hiyo kutekeleza takwa la kisheria na kuongeza kuwa taasisi na asasi hizo 743 ni orodha ya awali kwani uchambuzi unaendelea.
Amesema, “na hii ni orodha ya awali, uchambuzi wa taasisi zaidi unaendelea lengo ni kuhakikisha wadhamini wa taasisi zote wanatekeleza majukumu yao kikamilifu kwa mujibu wa sheria, katiba na maslahi mapana ya taifa, kushindwa kutekeleza takwa hilo ni kwenda kinyume na sheria na hatua dhidi yao zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kufuta bodi husika.”
Anatory ameeleza kuwa, sheria ya Muunganisho wa Wadhamini Sura ya 318, toleo la 2002 kifungu 23(1) (d) kinatoa maelekezo ya taasisi zote nchini zilizosajiliwa na Rita kufanya marejeo kwa mujibu wa sheria hiyo na kwamba bodi hizo zina jukumu la kuwasilisha marejesho kwa msimamizi mkuu wa wadhamini kila baada ya miezi 12.