Bodi ya filamu Tanzania imeahidi kuendeleza ushirikiano na wadau wa sekta ya filamu kuhakikisha sekta hiyo inakuwa chachu ya maendeleo nchini.

Ahadi hiyo imetolewa na Katibu Mtendaji wa bodi hiyo Joyce Fissoo wakati akifungua mafunzo ya uandishi wa miswada ya picha jongefu kwenye ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO leo jijini Dar-es-salaam.

Mafunzo hayo ya siku nne yamewezeshwa kwa ushirikiano kati ya Bodi ya Filamu Tanzania na Chama cha Waandishi wa Miswada ya Picha Jongefu Tanzania (TASA).

Kwenye hotuba yake Katibu Mtendaji wa Bodi hiyo alisisitiza umuhimu wa mswada kwenye utengenezaji wa filamu pale aliposema “mswada ni msingi wa filamu yoyote na mswada bora ndio utakao kuhakikishia filamu bora”.

Aidha ameupongeza uongozi wa Chama wa Waandishi wa Miswada ya Filamu Tanzania kwa kuandaa mafunzo hayo ambapo ameonyesha imani yataleta mabadiliko chanya kwenye ubora wa filamu za ndani.

Mbali na kuwapongeza viongozi wa chama hicho pia aliahidi kutoa ushirikiano wakati wowote atakapohitajika ili kuboresha tasnia ya filamu ncini. Kutekeleza kwa vitendo ahadi hiyo Fissoo alikubali kuwalipia ada ya uanchama washiriki wanane ambao walikuwa bado hawajajisajili kwenye chama hicho.

Mafunzo hayo ya siku nne yatakuwa ya vitendo na shirikishi ambapo yataongozwa na wakufunzi wawili kutoka nchini Marekani na yana lengo la kuwaongezea ujuzi waandishi wa miswada ya filamu wapatao 65 ili waweze kuandika miswada yenye ubora wa kimataifa.

Takwimu za Bodi ya Filamu Tanzania zinaonyesha jumla ya miswada 33 iliwasilishwa mwaka wa fedha 2014/2015 kati ya jumla ya filamu zaidi ya 1400 zilizokaguliwa. Idadi hiyo ni ndogo ukilinganisha na maombi 169 yaliyowasilishwa ndani ya mwaka huo kutoka kampuni za nje ambapo mamombi yote sawa na asilimia 100 yaliambatanishwa na miswada yake.

Kwenye risala yake Katibu wa TASA Christian Kauzeni alizitaja baadhi ya changamoto wanazokumbana nazo wanachama wao ni pamoja ukosefu wa sera ya filamu, wanachama kushindwa kujua wajibu wa mamlaka zinazosimamia sekta ya filamu kama vile COSOTA, Bodi ya Filamu Tanzania,

Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA)na kukosekana kwa mfumo yakinifu wa elimu kwa waandishi wa miswada ya filamu. Bi. Fissoo aliahidi kuzishughulikia changamoto hizo.

 

Mwanasheria Mkuu Avitaka Vyama Vya Siasa Kufuata Misingi Ya Katiba, Sheria Na Busara
Picha: Ziara ya Majaliwa Nairobi