Bodi ya Filamu nchini Tanzania imeonyesha kusikitishwa na kauli ya Mbunge wa Geita Vijijini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Joseph Musukuma aliyoitoa wakati akichangia hoja katika bajeti ya Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo iliyowasilishwa na Waziri wa Habari Dkt. Harrison Mwakyembe.
Katika taarifa iliyotolewa na bodi ya filamu nchini Tanzania, imelaani vikali kauli hiyo na kumtaka mbunge huyo wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma kujikita katika hoja za kuisaidia Tasnia ya Filamu nchini na siyo kuidhalilisha.
”Rai yetu kwa wasanii wa filamu nchini, tusimame kwa umoja wetu kulaani kauli hizi kwani zinaichafua na kudhalilisha tasnia ya filamu nchini Tanzania,”Imeeleza taarifa hiyo iliyotolewa na bodi ya filamu
Aidha, akichangia hoja mara baada ya uwasilishwaji wa bajeti ya Wizara ya Habari Sanaa Utamaduni na Michezo, Aprili 18, 2019, mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma alisema kuwa Tasnia ya Filamu ncnini ipo hoi taabani, huku akisema kuwa wasanii wa Bongo Movie hawana kitu wanategemea michango ya misiba, kufungua madanguro na kuwa makuwadi wa wanaume.