Bodi ya mikopo ya elimu ya juu HESLB imetoa taarifa kwa wadau wote kuwa kuwa leo Alhamisi Septemba 10, 2020, saa 6:00 usiku dirisha la upokeaji wa maombi ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2020/2021 kwa njia ya mtandao, litafungwa rasmi.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru, imeeleza kuwa baada ya muda huo, usajili mpya kwa ajili ya maombi mapya hautaruhusiwa.

Tarehe 21 Julai, mwaka huu, HESLB ilifungua dirisha la maombi ya mkopo kwa njia ya mtandao na kisha kufuatia maombi ya wazazi, walezi na wanafunzi, muda wa maombi ya mkopo uliongezwa kwa siku 10 hadi leo Septemba 10, 2020 saa sita usiku.

Badru ameeleza kuwa mpaka mchana wa leo, jumla ya maombi 92,947 yamesajiliwa na kupokelewa yakiwemo maombi 7,500 yaliyopo katika hatua mbalimbali za ukamilishwaji.

HESLB inatoa wito kwa waombaji mikopo 7,500 wenye maombi yasiyokuwa na viambatisho muhimu, kukamilisha maombi hayo haraka iwezekanvyo ili yaweze kujumishwa kwenye tathmini na uchambuzi.

Uhakiki wa taarifa za maombi ya mikopo, utaanza tarehe 1 Oktoba na kisha HESLB itaorodhesha maombi yaliyobainika kuwa na kasoro mbalimbali kupitia katika mfumo.

Kwa kuzingatia kuwa mchakato wa maombi ya mikopo unahusisha wadau mbalimbali, HESLB inawasisitiza wadau inaoshirikiana nao ikiwemo Shirika la Posta Tanzania (TPC) kuendelea kuwahudumia waombaji mikopo wote kwa kupokea na kutuma maombi yao kwa kuzingatia mwongozo wa uombaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2020/2021.

Serikali kupitia HESLB, imetenga kiasi cha TZS Bilioni 464 kwa ajili ya wanafunzi 145,000, ambapo kati yao wanafunzi wanufaika 54,000 watakuwa wa mwaka wa kwanza na 91,000 ni wanafunzi wanufaika wanaoendelea na masomo.

Aidha, bodi imewashauri wazazi, walezi na wanafunzi kuendelea kufuatilia vyanzo rasmi ikiwemo tovuti ya HESLB (www.heslb.go.tz) kuhusu taarifa muhimu na orodha ya watakaopangiwa mikopo kwa mwaka wa masomo 2020/2021 na kwa mujibu wa kalenda ya mwaka wa kitaaluma (academic almanac) ya mwaka huu.

Basi la Isamilo lapata ajali Mbeya
TRA kupita mlango kwa mlango