Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza kufungua dirisha la maombi ya mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya juu kwa mwaka 2021/2022 linatarajia kufunguliwa Julai Mosi mwaka huu.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa hati ya makubaliano baina ya HESLB na Wakala wa Usajili, Ufiilisi na Udhamini (RITA) iliyofanyika leo Juni, 7, 202, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema kabla ya kufunguliwa kwa dirisha la maombi HESLB, itatoa mwongozo wa uombaji mikopo unaotarajiwa kutolewa Juni 25 mwaka huu.

“Tunawasihi wanafunzi kusoma kwa makini mwongozo wa uombaji mikopo utakaopatikana katika tovuti yetu (www.heslb.go.tz) ambao utachapishwa katika lugha ya kiingereza na Kiswahili, kabla ya kufungua dirisha la maombi mwanafunzi anapaswa kusoma mwongozo huu” amesema Badru.

Aidha amesema kuwa katika mwaka wa masomo 2021/2022 Serikali imetenga kiasi cha TZS 500 Bilioni kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu inayotarajia kunufaisha jumla ya wanafunzi 160,000.

Kwa upande wa urejeshaji mikopo, Badru amesema hadi kufikia mwezi Mei mwaka huu, HESLB imekusanya kiasi cha TZS 168 Bilioni, ambayo ni sawa na 88.4% ya lengo la kukusanya TZS 190 Bilioni katika mwaka wa fedha 2020/2021.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mtendaji wa RITA, Emmy Hudson amesema Ofisi imekamilisha hatua mbalimbali za kuwawezesha wanafunzi wahitaji ikiwemo kutoa mwongozo wa uhakiki wa Vyeti vya kuzaliwa ambavyo ni moja ya nyaraka muhimu zinazohitaji wakati wa kuomba mikopo.

Ameongeza kuwa RITA itafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na kuimarisha ushirikiano na HESLB ikiwemo kuimarisha mifumo ya Tehama inayolenga kuondoa changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafunzi wakati wa uombaji mikopo ya elimu ya juu.

Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ni mali ya Serikali - Ndugulile
Mchakamchaka wa RC Makalla Dar