Serikali imesema kuwa kuanzia Julai Mosi mwaka huu Bodi ya Mikopo (HESLB), itafuta tozo ya asilimia 6 ya kulinda thamani ya fedha inayotozwa kwa wanufaika wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Kauli hiyo imetolewa leo Mei 25, 2021, Bungeni Dodoma na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Juma Omary Kipanga wakati akijibu swali la Mbunge wa Mtambwe Khalifa Mohammed Issa lililohoji ni lini serikali itapeleka Bungeni muswada wa mabadiliko ya sheria ya mikopo ya elimu ya juu.

“Kuanzia Julai 1, 2021, Bodi ya Mikopo itafuta tozo ya 6% ya kulinda thamani ya fedha inayotozwa kwa wanufaika wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu,” amesema Kipanga.

“Vilevile itatekeleza maelekezo yangu ya kuondoa tozo ya asilimia 10 kwa wanufaika wanaochelewa kurejesha mkopo baada ya muda wa miezi 24 kupita baada ya kuhitimu,” ameongeza Kipanga akijibu swali hilo.

Kufutwa kwa tozo hizo ni utekelezaji wa agizo lililotolewa hivi karibuni na Rais Samia Suluhu Hassan ambapo aliagiza kuondolewa kwa tozo hizo ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kuwaumiza wahusika ambao ni wale waliokuwa wanufaika wa bodi ya mikopo wakati wanasoma.

Wizara ya Mambo ya Ndani yavalia njuga kukomesha uhalifu
Majambazi Dar wauona moto wa RPC mpya