Wanafunzi na wadau mbalimbali wameilalamikia Bodi ya Mikopo kwa kuweka vigezo vigumu bila ya kuwafikilia kwa undani watu wanaotaka kufaidika nayo.
Katibu wa Mtandao wa Wanafunzi nchini (TSNP), Joseph Malecela amesema kuwa katika utoaji wa mikopo hiyo kumekuwa na ubaguzi na upendeleo kwa baadhi ya michepuo ya wanafunzi hasa wanaosomea Sayansi huku wengine wakikosa kabisa.
Malecela amesema ni vyema Bodi ya Mikopo itoe ufafanuzi zaidi juu ya kifungu cha muongozo wa kuomba Mkopo Na 1.0 (vii) ambacho kinasema waombaji ambao wazazi au walezi ni wamiliki wa biashara, mameneja wakubwa katika mamlaka zinazotambulika zenye usajili, hawaruhusiwi kuomba mkopo.
“Sisi tunachojiuliza kama Mtandao wa wanafunzi Tanzania kwamba tuna mfumo gani wa mkopo ambao unaweza kupima kiwango cha uwezo wa mzazi katika kuweza kumudu hizo gharama, na madodoso gani yamewekwa ili kujua huyu mtu anafanya biashara kubwa hata kama si Meneja mkubwa”, amesema Malecela.
Hata hivyo, kwa upande wake Afisa Mawasiliano Mwandamizi kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Veneranda Malima amesema kuwa kifungu hicho kipo sawa na hawawezi kusema kwamba kitaondolewa.