Bodi mpya ya Ushauri ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) imezinduliwa kwa lengo la kuimarisha ufanisi wa Taasisi na uangalizi wa karibu katika matumizi ya fedha za umma katika mahitaji mbalimbali.
Uinduzi huo umefanywa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji mjini Singida ambapo amesema Bodi hiyo itamsaidia Waziri wa Fedha na Mipango kupata ushauri wa kitaalam na hatimaye kutoa maamuzi yenye tija kwa Taasisi na Taifa kwa ujumla.
“Bodi hii ya Ushauri inategemewa kutoa mchango wa mawazo na kitaalam yanayohusu uendeshaji na uboreshaji wa Taasisi yetu ya TIA ili kuendana na mabadiliko yanayoendelea duniani katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kiteknolojia, kisiasa na kijamii”, amesema Dkt. Kijaji.
Aidha, ameongeza kuwa Bodi hiyo ina wajibu wa kujua ubora wa wanafunzi wanaohitimu katika chuo hicho ikiwa ni pamoja na ubora wa vyeti vyao kuendana na uwezo wao wa kufanya kazi katika fani walizosomea na kukabiliana na changamoto kwenye maeneo ya kazi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania, Said Chiguma amesema Taasisi hiyo inakabiliwa na changamoto ya uchache wa miundombinu kama vile kumbi za mihadhala, madarasa, maktaba na maabara za kompyuta ambavyo ni nyenzo muhimu katika utoaji wa elimu iliyo bora.
-
Rais Magufuli: Aliyemuita Kafulila tumbili yeye ndiye tumbili kwa IPTL
- Majaliwa amtumbua DED wa mbozi kwa matumizi mabaya ya fedha za umma
Taasisi ya Uhasibu Tanzania ni chuo cha Serikali ambacho kinatoa mafunzo katika fani za Uhasibu, Ununuzi na Ugavi, Usimamizi wa Biashara, Uongozi wa Rasilimali Watu, Masoko na Uhusiano wa Umma pamoja na Uhasibu wa Fedha za Umma kuanzia ngazi ya Astashahada (Certificate), Stashada (Diploma) na Shahada(degree)