Bodi ya Shirika la Ndege la Msumbiji imevunjwa baada ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Carlos Agostinho do Rosário pamoja na abiria kadhaa kukosa ndege wakilazimika kusubiri kwa muda mrefu kwenye uwanja wa ndege jijini Maputo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari vya nchi hiyo, Waziri Mkuu aliyeambatana na viongozi wengine alielezwa kuwa ndege aliyokuwa amepangiwa haikuwa na mafuta.
Imeelezwa kuwa ukosefu wa mafuta ulitokana na mgomo wa kampuni iliyokuwa ikiwauzia mafuta iliyodai kuwa inahitaji kulipwa kwanza kabla ya kutoa huduma kutokana na mgogoro wa rundo la madeni dhidi yake.
Kumekuwa na mgomo baridi wa makampuni yanayosambaza mafuta kwa shirika hilo la ndege kwa kipindi cha siku tatu, hali iliyozua taharuki na usumbufu kwa abiria.
Baada ya kuvunjwa kwa Bodi hiyo, menejimenti imetoa tamko ililitaja tukio la kumchelewesha Waziri Mkuu na kumfanya aungane na abiria wengine kuhangaika kupata ndege kuwa ni tukio la aibu, kwa mujibu wa BBC.
Shirika hilo limeomba radhi wateja wake na kuwataka kupiga simu ili kufahamu taarifa za mabadiliko ya ndege.
Ndege za Shirika hilo la Msumbiji zilipigwa marufuku kufanya safari zake katika nchi za Umoja wa Ulaya mwaka jana. Sababu za marufuku hiyo ilielezwa kuwa ni kukosa uangalizi makini.