Ndege aina ya 737 MAX ya kampuni ya Boeing yenye makao makuu Marekani, imepaa angani kwa mara ya kwanza baada ya ajali mbili kubwa zilizosababishwa na hitilafu za kiufundi kutokea.
Ndege aina ya Boeing 737 Max zilipigwa marufuku kupaa angani kufuatia ajali mbili kubwa ambazo zilisababisha vifo vya watu zaidi ya 300.
Mwaka 2018 watu 189 walifariki katika ajali ya ndege aina ya Boeing 737 Max iliyoanguka nchini Indonesia na mwaka 2019 watu 157, pia walifariki kwenye ajali nyingine ya ndege ya Boeing iliyoanguka nchini Ethiopia.
Baada ya ajali hizi mbili kubwa kutokea, ndege zote za 737 MAX zilipigwa marufuku ya kusafiri kote ulimwenguni.
Baada ya uchunguzi uliochukua miezi 20, Shirikisho la Usafiri wa Anga la Marekani lilitangaza kutatua hitilafu zilizokuwa katika ndege hizo.
Marufuku ya kusafiri iliondolewa mwezi uliopita, na ndege hizo zikatangazwa kuwa salama na ndege ya Boeing 737 MAX ilipaa kwa mara ya kwanza.
Abiria wa kwanza wa ndege hiyo walikuwa wawakilishi wa vyombo vya habari ambapo ndege ya kwanza ilisafiri kutoka Dallas kwenda Tulsa, Oklahoma, safari ambayo ilitekelezwa bila matatizo.
Ndege ya abiria aina ya Boeing 737 MAX itatekeleza safari yake ya kwanza ya kibiashara tarehe 29 Desemba, mwaka huu.