Kampuni ya Boeing imetangaza kuwa itasimamisha kwa muda uzalishaji wa ndege zake zilizokumbwa na matatizo za 737 Max kuanzia Januari 2020.
Uzalishaji wa ndege hizo ulikuwa ukiendelea licha ya ndege hizo kuzuiwa kupaa kwa miezi 9 sasa baada ya kuhusika katika ajali mbili zilizosababisha vifo vya mamia ya watu.
Ambapo zaidi ya watu 300 walipoteza maisha wakati ndege mbili za 737 Max zilipoanguka nchini Indonesia na Ethiopia baada ya kuripoti matatizo katika mfumo wake mpya.
Kampuni ya Boeing ilikua ikitumaini kuwa ndege hizo zitarejea tena angani kufikia mwishoni mwa mwaka huu lakini wasimamizi wa safari za anga nchini Marekani wamesema ndege hizo hazitapewa kibali cha kurejea angani katika siku za hivi karibuni.
Aidha kampuni hiyo imesema katika taarifa yake kwamba haitawafuta kazi wafanyakazi waliopo wa ndege za 737 Max, lakini kusimamishwa kwa utengenezaji kunaweza kuwaathiri wasambazaji na uchumi kwa ujumla.