Kundi la kigaidi la Boko Haram limeripotiwa kufanya mashambulizi katika eneo la Maiduguri nchini Nigeria na kuua watu 15.
Afisa wa wakala wa kitengo cha dharura cha taifa amewaambia waandishi wa habari kuwa watu wengine 68 wamejeruhiwa vibaya katika shambulizi hilo, kwa mujibu wa BBC.
Shambulizi hilo ni kinyume cha hatua iliyotangazwa na Serikali ya nchi hiyo kuwa wako mezani wakifanya majadiliano na kundi hilo la kigaidi.
Maiduguri imekuwa kitovu cha mashambulizi ya Boko Haram kwa miaka tisa ambapo limesababisha vifo vya watu zaidi ya 20,000.
Rais Muhammadu Buhari amewahi kuripotiwa akisema kuwa kundi hilo limesambaratishwa na vikosi vya Serikali, lakini miezi kadhaa baadaye likaibuka tena.
Vyanzo vya jeshi la Nigeria vimeeleza kuwa shambulizi hilo lilifanyika Jumapili karibu na eneo la kambi ya jeshi.
“Watu 68 wamejeruhiwa, 15 wasio na hati wameuawa,” alisema Bello Dambatta, mwenyekiti wa wakala wa kitengo cha dharura cha taifa ‘State Emergence Management Agency (SEMA).