Kundi la kigaidi la Boko Haram limevamia vijiji vitatu Kaskazini-Mashariki mwa Nigeria na kuua watu kumi na wawili, Jumapili.
Wakaazi wa vijiji hivyo vya Dala-Melari, Fuguri na Femari pamoja na maafisa wa jeshi la Nigeria wamekaririwa na AFP wakieleza kuwa uvamizi huo mbali na mauaji umeacha majeruhi kadhaa.
“Wapiganaji wa Boko Haram walifyatua risasi na kuwalazimisha watu wote kukimbia nje ya vijiji vyetu,” Ibrahim Limam anakaririwa.
Wanakijiji hao walielekeza lawama zao kwa kiongozi wa Boko Haram, Abubakar Shekau kwa kuamuru mashambulizi hayo.
“Watu waliuawa na wengine wamejeruhiwa. Walichoma vijiji vyote na kuharibu vyakula ikiwa ni pamoja na mashamba,” aliongeza Limam.
Maafisa wa Jeshi la Nigeria ambao hawakutaka kutajwa wamekaririwa pia wakieleza kuwa wanamgambo hao walivamia vijiji hivyo majira ya saa nne usiku.
“Waliiba vyakula vyetu vyote na kuchoma vilivyobaki. Waliwaua watu wetu kumi na wawili na kuwaachia raia majeraha makubwa,” alikariri mmoja.
Mratibu wa Wakala wa Taifa wa Kushughulikia Dharura (NEMA) wa Kanda ya Kaskazini-Mashariki, Bashir Garga alisema kuwa takribani wanakijiji 1,300 waliyakimbia makazi yao katika tukio hilo. Alisema mbali na bunduki, Boko Haram walitumia mapanga kuua wakulima.
Ndani ya kipindi cha miaka 9, kundi la Boko Haram limeripotiwa kuua watu 27,000 na kusababisha watu wengine takribani milioni 2 kuyahama makazi yao. Kundi hilo pia limeanza kuleta machafuko kwenye mipaka ya nchi za Chad, Niger na Cameroon.