Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amesema kuwa amefurahishwa na utendaji kazi wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa jinsi lilivyorudi kwa kasi na kuanza kupata mafanikio huku naye akisema yupo mbioni kulifufua shirika lao.
Museveni ameyasema hayo alipokuwa nchini Tanzania kwa ajili ya shughuli ya uwekaji wa jiwe la msingi kwenye mradi wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Hoima nchini Uganda, mpaka Tanga Tanzania, na kusema kuwa anaipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada za kurudisha ATCL.
“Tunataka kutoa hongera kwa Watanzania, tunasikia mmerudisha kampuni yenu ya ndege, na sisi hivi karibuni tutafufua shirika letu la ndege, kwa hiyo hizi kampuni za ndege tutafaidika kwa kutumia mafuta ambayo hayapo kwenye gharama kali,” amesema Museveni
Hata hivyo, Shirika la ndege la Tanzania lilikufa kwa miaka mingi, lakini baada ya kuingia Rais Magufuli alilifufua, na mpaka sasa linafanya kazi likiwa na ndege tatu, huku shirika la ndege ATCL likitarajia kuleta ndege zingine kubwa aina ya Boeing 787 Dash 8 Dreamliner.