Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amesema ndege ya Tanzania aina ya Bombardier Q400 imekamatwa nchini Canada.
Profesa Kabudi ameyasema hayo leo, Novemba 23, 2019 Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma wakati Rais John Pombe Magufuli alipokuwa akiwaapisha mabalozi wapya.
Amesema kuwa aliyesababisha ndege hiyo kushikiliwa ni yuleyule, Hermanus Stayn raia wa Afrika Kusini aliyekuwa amefungua kesi na kusababisha ndege ya Tanzania aina ya Airbus A220-300 kushikiliwa nchini Afrika kusini, Agosti mwaka huu.
Amesema baada ya Tanzania kushinda kesi ya msingi na rufaa aliyoikata, ameamua kukimbilia Canada ambapo amesababisha Bombardier Q400 kukamatwa, na kwamba hiyo inatokana na hujuma wanazozifanya wasioitakia mema Tanzania.
“Juzi limetokea jambo la kusikitisha ambalo ni vyema watanzania pia walielewe jinsi ambavyo hujuma za kibeberu zikifanyika kurudisha kasi ya maendeleo, tena kwa mara ya tatu ndege ambayo ilitakiwa kufika Tanzania imekamatwa tena Canada na kesi ipo mahakamani na aliyefanya hivyo ni mtu yuleyule aliyekamata ndege yetu Afrika Kusini, tukaenda mahakamani tukamshinda; sasa amekimbilia Canada na amekamata Ndege yetu ya Bombadier Q400,” amesema Waziri Kabudi.
Katika hatua nyingine Profesa Kabudi amemshauri Rais Magufuli, kama ikiwezekana waache kununua ndege nchini Canada kwakuwa mara nyingi ndege zimekuwa zikikamatwa nchini humo, lakini zinazotoka Marekani zinafika salama .
“Jana nimemuita Balozi wa Canada na alifika Dodoma na nimemuambia kinagaubaga na bila tashwishwi kwamba hatufurahishwi kabisa kwa tabia na vitendo hivi vya kila ndege yetu inapotakiwa kuondoka Canada kurudi Tanzania inakamatw,” alisema Profesa Kabudi.
“Kwa maana hiyo tunafikiri Mhe Rais kukushauri kama Canada inaendelea kuruhusu vitu hivi sio wao pekee wanatengeneza ndege, hatukufanya makosa kwenda kununua kwao hata Brazil wanatengeneza ndege,” ameongeza.
Waziri Kabudi ameongeza kuwa tayari hatua zote za kimahakama zimekwishachukuliwa ili kuweza kuikomboa Ndege hiyo.